Friday, December 7, 2012

Mnyika aibuka Kidedea, Slaa Atakiwa Kujiuzuru

 
ALIYEKUWA mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa 2010,  Hawa Ng’humbi jana ameondoa rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka juzi yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo hilo John Mnyika.
Rufaa hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa jana katika Mahakama ya Rufaa Kanda ya Dar Es Salaam mbele ya jopo la Majaji watatu, Jaji Salum Massati, Jaji Nathalia Kimaro na Jaji Catherine Urio.
Hata hivyo, Ng’humbi kupitia kwa Wakili wake Issa Maige aliiomba Mahakama hiyo kuondoa rufaa hiyo kwa madai kuwa ameshakubaliana na mrufani wake (Mnyika).
Kutokana na ombi hilo la upande wa mrufaa, Kiongozi wa jopo hilo la Majaji, Jaji Urio alisema Mahakama imefuta rufaa hiyo.
Ng’humbi alifungua kesi akipinga matokeo ya uchaguzi  mkuu wa mwaka juzi yaliyompa ushindi Mnyika kwa madai kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi katika uchaguzi huo.
Mei 24 mwaka huu, Jaji Upendo Msuya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam alitupilia mbali maombi ya Ngh’umbi na kuthibitisha Mnyika kuwa Mbunge halali wa Jimbo la Ubungo.
Jaji Msuya alisema Ng’humbi alishindwa kuthibitisha madai yake na kuonesha jinsi yalivyoathiri matokeo ya uchaguzi huo na kutangaza kuwa uchaguzi huo ulikuwa halali na kumtaka alipe gharama za uendeshaji wa kesi.
Ng’humbi alikuwa na hoja tano ambazo ni Mnyika alimtuhumu kuuza nyumba za Umoja wa Wanawake (UWT) , Kutumia Laptop za Mnyika kuhesabu kura, kuingia watu wengi wa Chadema katika chumba cha kuhesabia kura, kuwepo kwa  kwa kura hewa 16,000 na kukosewa kwa karatasi za kujumlisha kura (form).
Katika hukumu hiyo Jaji Msuya alisema, mashahidi wa Ng’humbi hawakuonesha wala kuthibitisha madai yaliyowasilishwa yalitendeka vipi na ni namna gani yaliathiri matokeo ya uchaguzi.
Katika madai kuwa zaidi ya kura 14,000 alizodai hazieleweki zilitoka wapi Jaji alisema alihesabu kura hizo walizopata wagombea wa vyama 16 na kubaini ni kosa tu la kibinadamu na halina uhusiano wowote na Mnyika.
Akizungumza nje ya Mahakama baada ya uamuzi huo wa Mahakama, Mnyika alisema kwasababu mahakama hiyo ndiyo ya mwisho kuondolewa kwa rufaa hiyo kunathibitisha alishinda kihalali na yeye ni Mbunge halali wa jimbo hilo kama ilivyothibitishwa katika Mahakama Kuu.
Alisema, siku chache zilizopita  wakili Maige aliwasiliana na  wakili wake Edson Mbogoro  akiomba  kuondoa rufaa hiyo  mahakamani na kusamehewa gharama za uendeshaji wa rufaa hiyo.
Mnyika alisema amemsamehe Ngh’umbi kulipa gharama za uendeshaji wa rufaa hiyo lakini gharama za kuendesha kesi ya msingi ambayo hukumu yake ilitolewa Mahakama Kuu bado iko pale pale.
Aliongeza kuwa licha ya kuwa kesi hiyo ilichukua miaka miwili  tangu ilivyofunguliwa mwaka juzi aliendelea kuwatumikia wananchi bila kujali kama kuna kesi mahakamani.
Wafuasi wa Chadema walikuwa wamefurika nje ya mahakama hiyo wakionesha ishara yao ya kunyoosha vidole viwili hewani huku wengi wao wakisema wamefurahishwa sana na uamuzi wa Ngh’umbi kwa kuwa walimchagua mbunge huyo kihalali.
Walitoka katika eneo hilo wakiandamana,  hata hivyo walipofika katika maeo ya Posta mpya Mkuu wa Kituo cha Kati cha Polisi , Suzana Kaganda aliwataka kutawanyika katika eneo hilo kwa kuwa hawakuruhusiwa kufanya maandano kutokana na ugeni uliopo nchini kwa sherehe za Uhuru.
Mnyika aliwataka wafuasi hao kutii amri hiyo na hivyo walitawanyika na wengine walipanda daladala.
Katika hatua nyingine, Mjumbe  wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Eddo Mwamalala, amedai kitendo cha Katibu Mkuu wa Chama hicho Taifa Dk Wilbroad Slaa kukiri kuwa anamiliki kadi ya CCM kimewadhalilisha huku akimtaka ajiuzuru wadhifa alionao kwa ajili ya kulinda maslahi ya chama hicho.
Mwamalala ambaye amewahi kuwa Katibu wa Chama hicho katika Mkoa wa Mbeya kabla ya kusimamishwa nafasi hiyo na Dk. Slaa alisema kitendo hicho kinaonesha wazi namna kiongozi huyo alivyokosa uadilifu na huruma kwa Watanzania walioweka rehani maisha yao ili kuliletea Taifa maendeleo.
Akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari Jijini Dar es salaam jana, Mwamalala alisema kwa kufanya hivyo, Dk Slaa pia anakuwa amekiuka sura ya tano ibara ya kwanza ya Katiba ya Chama hicho inayomtaka mwanachama yeyote wa chama hicho kutokuwa mwanachama wa chama kingine baada ya kujiunga na Chadema.
“Dk Slaa ni kiongozi na jicho la Chadema, kitendo cha yeye kukiri hadharani kuwa anamiliki kadi ya CCM, kimekitia doa chama chetu na kinaonesha udhaifu tulionao hivyo kwa maslahi ya chama hiki ni vizuri akajiuzuru na kuwapisha watu wenye sifa ya kuwa viongozi wa kweli katika chama,” alisema Mwamalala.
Hivi karibuni, Slaa kupitia mkutano wake na waandishi wa habari, alikiri kumiliki kadi ya CCM baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye kutamka hadharani kuwa Katibu huyo wa Chadema anamiliki kadi ya CCM.
Kutokana na kitendo hicho cha Dk Slaa, Mwamalala alisema ni ni vyema Katibu huyo akajitathimini mwenyewe kama anatosha kuendelea kuongoza chama na wanachama wakati anavunja na kudharau Katiba yake.
“Nawaomba Watanzania wote wanaoiunga mkono Chadema, tuungane kwa pamoja kama kweli tumedhamiria kushika dola Mwaka 2015, watu kama Dk Slaa ni ndumilakuwili hawatufai tena bali wapo wakitumia shida za wananchi kujipatia umaarufu wa kuendesha maisha yao huku wakiacha wananchi wakiteseka,” alisema Mwamalala.
 

0 comments:

Post a Comment