MAONESHO ya 13 ya Nguvu Kazi/Jua Kali kwa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), yamefunguliwa juzi mjini hapa
huku Makamu Spika wa Bunge la Burundi, Jean Kabura akisema maonesho hayo yana
nia ya kuendeleza shughuli za sekta binafsi na kuongeza ajira kwa wajasiriamali.
Kabura
alisema maonesho haya yanaendana na sera ya Afrika Mashariki ya kuendeleza
viwanda ambayo ilipitishwa na Wakuu wa Nchi Wanachama katika mkutano wao wa
kilele mwaka 2011 mjini hapa.
Aidha,
ameongeza kuwa maonesho haya yatawasaidia vijana kujikita katika sekta isiyo
rasmi ili kuongeza ajira kwa vijana na
hatimaye kuondoa kabisa umasikini wa kipato.
Makamu
Spika aliwaomba wafadhili kuangalia bidhaa za wajasiriamali ili kutafuta njia
za kuwasaidia kuongeza ubora wa bidhaa hizo na kuwatafutia masoko. Aliwashukuru
waandaji wa maonesho kwa maandalizi mazuri na kufanikisha shughuli nzima ya
uzinduzi.
Akitoa
salamu kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi wa
Tanzania nchini Burundi, Dk James Nzagi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya
Burundi kwa maandalizi mazuri ya maonesho na kwa mapokezi mazuri kwa washiriki
wote waliofika Bujumbura.
Aidha,
aliwashukuru watumishi wa mipakani kwa ushirikiano waliouonesha kwa
wajasiriamali wa Tanzania kupita kwa usalama na mali zao bila kusumbuliwa na
kusema kuwa hii ni ishara ya kuonesha ushirikiano ulio imara katika nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Dk
Nzagi alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayachukulia
maonesho haya kama njia ya kubadilisha Tanzania kuwa taifa la uchumi wa kati na
unaoendeshwa na viwanda.
Alisema
kwa kuzingatia umuhimu wake kwa Watanzania, Serikali imeendelea kuwasaidia
wajasiriamali wa sekta isiyo rasmi kushiriki maonesho haya ili kukuza shughuli
zao na kuimarisha ajira zao.
Katika
maonesho haya, Tanzania ilipewa nafasi 185 za wajasiriamali kushiriki.
Wajasiriamali 87 ndio walioshiriki wakiwa na bidhaa mbalimbali ambazo ni pamoja
na nguo za batiki, vyakula vya kusindika, bidhaa za ngozi, dawa za asili, dagaa
wa kukaushwa, mafuta ya ubuyu na vikapu vya kushona.
Maonesho
ya 13 ya Nguvu Kazi/Jua Kali ya Afrika Mashariki hufanyika kila mwaka kwa
mzunguko katika kila nchi wanachama wa EAC baada ya kufunguliwa rasmi Novemba,
1999 mjini Arusha. Maonesho hayo kwa mwaka huu yanafanyika Burundi ikiwa ni
mara ya kwanza kufanyika nchini humo.
Maonesho
hayo yana lengo la kukutanisha wajasiriamali wadogo kwa ajili ya kubadilishana
uzoefu, kuwajengea mtandao wa kibiashara, kukuza vipaji vyao pamoja na
teknolojia.







0 comments:
Post a Comment