Monday, April 16, 2012

WANAFUNZI WAWEKANA KINYUMBA



 WANAFUNZI watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Tarime Mjini kwa tuhuma mbili tofauti za kutorosha wanafunzi wenzao na kukaa nao kinyumba.

Waliofikishwa mahakamani hapo jana ni Chacha Daud (18) anayesoma kidato cha nne na wenzake wawili wenye umri wa miaka 17 (majina yanahifadhiwa) mmoja wa kidato cha pili wa Sekondari ya Nkende na mwingine wa kidato cha pili wa Sekondari ya Nyamisangura.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Aminia, alidai mbele ya Hakimu Samwel Gimeno kuwa Aprili 12 saa mbili usiku katika kitongoji cha Msati, Chacha na mwenzake walimtorosha mwanafunzi
wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) na kuishi naye kinyumba, jambo lililofanya ashindwe kuhudhuria masomo.

Watuhumiwa wote wawili walikana mashitaka na kupelekwa rumande baada ya kushindwa
kupata dhamana iliyowataka kuwa na wadhamini wawili wenye mali isiyohamishika kila mmoja. Kesi yao itatajwa mwezi ujao.

Katika kesi nyingine, mwanafunzi wa Nyamisangura, alifikishwa katika Mahakama hiyo akidaiwa kumtorosha mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 15 wa Sekondari ya Nkende (jina linahifadhiwa).

Aminia alidai mbele ya Hakimu Gimeno kuwa Aprili 12 saa mbili asubuhi, alimtorosha mwanafunzi huyo na kwenda kuishi naye kinyumba.

Mwanafunzi huyo alikana mashitaka, ingawa binti huyo alisisitiza kuwa kushindwa kwake kwenda shule, kulitokana na kutoroshwa na mtuhumiwa huyo ambaye alirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hadi kesi hiyo itakapotajwa mapema
mwezi ujao.

Wakati huo huo, Blenda Stanley (18) alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na tuhuma za kumwibia mjomba wake redio na simu ya mkononi vyote vikiwa na thamani ya Sh 350,000.

Mshitakiwa alikana mashitaka na kupelekwa rumande baada ya kukosa dhamana


Source: Habari Leo

0 comments:

Post a Comment